Na RM
Jumanne, Desemba 24, 2024
Kipute cha fainali ya Mashindano ya kuwania taji la Funyula Sports Fest, katika kitengo cha soka, kitakutanisha timu ya NYSA FC na Lake View FC kitakachopigwa Jumatano hii ya Desemba 25, 2025 katika Kaunti ya Busia nchini Kenya.
Fainali hiyo ambayo inatarajiwa kuanza majira ya saa tisa alasiri, itapigwa kwenye Uwanja wa shule ya msingi ya Nandereka huko Bukiri ulioko eneobunge la Funyula.
Timu hizo zilitinga Fainali kutokana na kushinda mechi za Hatua ya Nusu fainali, zilizofanyika Jumanne ya Desemba 24, 2024. Lake View FC iliinyuka Bumbe FC mabao 2-1 katika Uwanja wa Busijo nayo NYSA FC iliishinda Reibentos FC mabao 4-3 kupitia mikwaju ya penalti kwenye Uwanja wa Luchululo.
Penalti za NYSA FC ziliwekwa kimiani na Titus Ochuli, Fidel Maiga, Franklin OJiambo na Shadrack Sianga. Nazo penalti za Reibentos FC zilifungwa na Ali Hassan, Brighton Oundo na Lamech Otieno.
Michuano hiyo ya mtoano ya Funyula Sports Fest ilianzia kwenye hatua ya Robo Fainali ikishirikisha timu nane.
Katika mechi hizo za robo fainali, Lake View FC iliichabanga Namuduru FC mabao 3-0 wakati NYSA FC ikaichuna Luchululo FC bao 1-0 nayo Bumbe FC iliilaza Sigalame FC bao 1-0 huku Reibentos FC ikatinga nusu fainali baada ya kuitandika Dragon FC bao 1-0.